Na Joan Lema
WAKATI Yanga ikiendelea na mchakato wa kumshawishi kiungo wao, Haruna Niyonzima kusaini mkataba mpya wa kuitumikia timu hiyo ambayo ni bingwa wa Ligi Kuu Bara, limeibuka jipya ambapo mchezaji huyo amepata ofa nono kutoka Tunisia.
Niyonzima ambaye amekuwa na msaada mkubwa klabuni hapo, bado hajasaini mkataba mpya mpaka sasa na anatarajiwa kuondoka nchini keshokutwa kwenda Rwanda kwa ajili ya kupumzika kabla ya kuamua kusaini Yanga au la.
Taarifa kutoka Tunisia zinaeleza kuwa, klabu moja kubwa ya nchini humo imeonyesha nia ya kumsajili Niyonzima ambaye ni kiungo wa zamani wa APR na tayari imeshampatia ofa nzuri ambapo mchezaji huyo amewajibu kuwa anaomba muda kuitafakari.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa Niyonzima ameshafanya mazungumzo na timu hiyo ya Tunisia lakini hajasaini makubaliano yoyote na viongozi wa Yanga wanahaha mchana na usiku kuhakikisha anasaini kabla ya kwenda Rwanda.
“Kila kitu kipo wazi, Yanga wanataka asaini kabla ya kuondoka kwenda kwao Rwanda, lakini yeye anataka asaini mkataba huo akiwa kwao kama alivyofanya awali wakati anatua Jangwani au pindi atakaporejea, Yanga wanajua akiondoka tu hawana chao tena.
“Watunisi wamemwambia kuwa watampa mshahara mzuri zaidi ya anaopata Yanga, pia wamemhakikishia kumpa nyumba na mazingira mazuri ya familia na kama ana mtoto au watoto watasomeshwa katika shule nzuri. Kilichobaki ni Niyonzima kukubali tu kwa kuwa muda wake wa kukaa Yanga umeisha,” kilisema chanzo.
Championi ijumaa lilipomuuliza Niyonzima juu ya taarifa hizo, alisema: “Kwa sasa sina haraka sana kusaini timu yoyote, nataka kupumzika kutokana na kwamba nimefanya kazi kubwa sana ya kuipatia timu yangu ubingwa.
“Kweli kuna timu ya Tunisia ambayo imeonyesha nia ya kunihitaji na imenipa ofa ambayo ni nzuri lakini bado sijasaini, hata timu yangu ya nyumbani ya APR nayo inanihitaji ila mimi bado ni mchezaji wa Yanga.
“Nahitaji kutuliza akili kabla ya kufanya maamuzi mengine yoyote kwa muda huu, mimi ni mwanadamu, nahitaji kupumzika kama wengine, hivyo naondoka naenda nyumbani kwa ajili ya kuitumikia timu yangu ya taifa na kupumzika,” alisema Niyonzima.
Source: Globalpublishers
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni